KATIKA toleo lililopita waandishi, David Meek na Tom Tyrrell walimwelezea kiungo Ryan Giggs wakati akiwa katika ubora wake na jinsi alivyoibeba Man United katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Arsenal na kuiwezesha kukata tiketi ya fainali ya michuano hiyo. Sasa endelea…
Ni mechi iliyohitaji kuchezwa kwa dakika za nyongeza, ilijaa ushindani wa kila aina, Beckham alifunga bao dakika ya 17, Bergkamp akaisawazishia Arsenal dakika ya 69, zikiwa zimebakia dakika chache mpira kumalizika Arsenal wakapata penalti, Schmeichel akaokoa na ndipo mechi ilipochezwa dakika za nyongeza.
Dakika 19 zikiwa zimepita, Giggs akiwa karibu na katikati ya uwanja aliwapangua mabeki kabla ya kuingia kati na kuujaza mpira wavuni.
“Sikuchoka, niliendelea kwenda mbele hadi nilipomwona David Seaman (kipa wa Arsenal) akiwa mbele yangu ndipo nilipofumua shuti kwa nguvu zote,’’ hivyo ndivyo Giggs alivyolizungumzia bao lake, uwiano sahihi wa kasi, mbinu na umaliziaji mzuri.
Katika Ligi Kuu England, Chelsea ilipoteza mwelekeo, ikaziacha Man United na Arsenal katika mapambano, wengi waliamini mechi zilizobaki zingekuwa sababu ya kuinyima United taji la tano, hata hivyo mambo yalikuwa tofauti kabisa na matarajio hayo ingawa adhabu za wachezaji ulikuwa ni mzigo usiohitajika wakati United ikielekea kuzuri.
Kasi ya kuwania mataji matatu ilidhihirika, lakini kwa Old Trafford kulizungumzia jambo hilo ilikuwa mwiko, hakuna mchezaji au ofisa yeyote anayehusika kwenye timu aliyekuwa na ruhusa wakati vyombo vya habari vikihoji na kuzungumzia mara kwa mara uwezekano wa kubeba mataji matatu.
“Juventus (kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya) watakuwa wenye kujiona wana nafasi na hivyo ndivyo ilivyokuwa hasa, yalikuwa ni matokeo mazuri kwao lakini watajuta kwa kuruhusu tuwafunge bao pekee dakika za majeruhi, nina matumaini makubwa kwamba tunaweza kucheza tena vizuri kama tulivyocheza kipindi cha pili na kutengeneza nafasi tatu au nne, ni kitu kinachoniambia kwamba tutakwenda kushinda,’’ ni kauli iliyotoka kwa Ferguson baada ya matokeo ya mechi yao ya kwanza ya nyumbani ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Juventus.
Katika mechi ya marudiano ya ugenini Turin ilionekana kama vile United walikuwa sahihi kwa kukaa kimya, baada ya dakika sita walikuwa nyuma kwa mabao 2-0, Filippo Inzaghi alifunga mabao mawili na kuiacha United ikihaha kujiweka sawa hasa baada ya kuwa nyuma kwa jumla ya mabao 3-1.
Kila kitu kilijionyesha kuwa dalili za kutolewa kwa masikitiko lakini Roy Keane alikuwa na mawazo mengine tofauti. Nahodha huyu kutoka Ireland alikuwa mwenye kuhamasika, akiongoza mashambulizi mbele alifunga bao moja dakika ya 24 kwa kichwa akiitumia kona ya David Beckham lakini furaha yake ilikuwa ya muda mfupi kwani dakika chache baadaye alipewa kadi ya njano kwa kumwangusha Zinedine Zidane. Akiwa tayari ana kadi nyingine katika mechi ya awali dhidi ya Inter Milan, hiyo maana yake ni kwamba kama United ingekwenda hadi hatua ya fainali Keane angeikosa hatua hiyo, majibu ya Keane katika hilo yalikuwa ni kuhakikisha wachezaji wenzake wanafikia hatua hiyo. United wakapeleka mashambulizi mbele na katika dakika ya 34, Yorke akachupa na kufunga bao la kichwa akiitumia vizuri krosi ya Beckham na mara wageni Man United wakawa wanautawala mchezo. Na kama matokeo yangebaki hivyo hivyo United wangekuwa wamefuzu fainali iliyokuwa inachezwa mjini Barcelona kwa faida ya mabao mawili ya ugenini.
Wakati mechi ikiendelea, United ilifanya mashambulizi makali mawili ingawa Wataliano nao hawakuwa nyuma, Inzaghi alifurukuta laki alinyimwa hat trick (mabao matatu) na kipa Schmeichel. Paul Scholes aliingia akitokea benchi na katika dakika nane tu za kuwa uwanjani alilimwa kadi, adhabu ambayo ilitosha kumfanya aikose mechi ya fainali mjini Barcelona.
Hofu hiyo mara moja ilisahaulika, zikiwa zimebakika dakika saba mpira kumalizika, Yorke aliingia katika eneo la hatari la Juventus kabla ya kuvutwa jezi na kipa. Mwamuzi bado kidogo atowe penalti lakini kabla ya uamuzi huo, Cole alijivuta na kuudokoa mpira hadi wavuni na kufanya matokeo yawe ya ushindi wa mabao 3-2 kwa Man United.
Martin Edwards, mwenyekiti wa klabu aliyelishuhudia tukio hilo alizungumzia maneno yafuatayo: “Nilikuwa na hofu baada ya matokeo kuwa 2-2 kwa sababu Juventus walihitaji bao moja tu ambalo lingewafikisha fainali lakini tulipogonga mwamba mara mbili nikaanza kujiwa na fikra za mataji matatu. Ni wazi kwamba ingekuwa jambo zuri kufanikisha hilo lakini bado nilikuwa na fikra kwamba jambo hilo lingekuwa ni miujiza.”